Aliyembaka binti wa miaka 9 na kumsababishia kifo wakati anajifungua akamatwa




Polisi nchini Zimbabwe imemtia mbaroni kijana wa miaka 26 Hatirarami Momberume kwa tuhuma za kumbaka mtoto ambaye baadaye aliaga dunia akijifungua . Binti huyo Anna Machaya amezikwa kwenye makaburi ya kidini huko Kusini mashariki mwa Zimbabwe.



Watetezi wa haki za binadamu wameunga mkono hatua hiyo ya Polisi ya kumkamata kijana huyo pamoja na wazazi wa binti huyo. Wanatuhumiwa kwa kukubali mtoto huyo tangu akiwa na miaka 9 kuwa mwenza wa mwanaume huyo na kudanganya kuhusu umri sahihi wa binti huyo.

Awali alitambulika kwa bahati mbaya kama Memory, huku hashtag ya JusticeForMemory ikisambaa kwenye mitandao mingi ya kijamii.

Kifo chake, kilichokuja siku chache baada ya Anna kufikisha miaka 15, kilizua hasira nchini humo kuhusu kuongezeka kwa vitendo vya ubakaji vilivyo nyuma ya pazia za ndoa za utotoni hasa zinazofungwa kwenye jamii za madhehebu kadhaa ya dini.

Hata hivyo wanaotenda vitendo hivyo ni nadra sana kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria huku Mamlaka wakiwemo wanasiasa wakituhumiwa kwa kufumbia macho vitendo hivyo .

Polisi wanasema uchunguzi kuhusu suala la Machaya unaendelea. Licha ya mahakama ya kikatiba nchini humo kuzuia ndoa za wanandoa walio chini ya umri wa miaka 18, bado ndoa hizo zinaendelea.